Kanisa la Mungu; Mpinga Kristo yuaja! Tupo, tunaendelea kuishi, lakini hatutaishi milele hapa duniani, kwa wale wenye ufahamu sisiti wala sina shaka yoyote kutamka bayana kwamba tupo tunamngoja Yesu ambaye punde, kwa ratiba za Kimbingu atatokea mawinguni. Nakuhakikishia, Yesu anarudi!
Tunapozungumza habari za kurudi kwa Kristo bado kuna wale wanaodhani kwamba tunafanya mizaha, au tunakamilisha tu ratiba za dini na madhehebu yetu, lakini sivyo ilivyo. Ni vile tu kwamba hatuna lugha ingine ya kueleza ukweli huu, laiti kama ROHO MTAKATIFU angetujalia, tungeitumia!
Ninao ujumbe kwako, na ujumbe wangu leo umesimamia katika andiko hili; Daniel 12:4, tusome hapo,
“Lakini, Ee Daniel, yafunge maneno haya, ukakitie muhuri kitabu, hata wakati wa mwisho, wengi wataenda mbio huko na huko, na maarifa yataongezeka”
Nimetangulia kusema, kwamba laiti kama tungekuwa na lugha zaidi ya hapa, lakini andiko hili tulilolisoma, kama ingekuwa ni kwa Kiswahili chetu cha leo lingesomeka hivi:-
“Lakini wewe, Ee Daniel, yafanye maneno haya kuwa mafumbo hata wakati wa mwisho, wengi watakuwa ‘busy’ na maarifa yataongezeka”
Fuatilia kwa makini yale maneno yaliyokolezwa kwa wino mweusi, utaona kwamba msisitizo uko katika maneno yafuatayo;
• maarifa yataongezeka
• wengi watakuwa ‘busy’
Katika zama zetu za leo huwezi kuzungumzia maarifa bila kuhusisha utandawazi, bila kuhusisha zama hizi za maendeleo ya sayansi, biashara na uchumi. Ukizungumzia maarifa utakuwa umegusia benki, upashanaji habari (mass communication) kupitia mitandao ya kompyuta, satelaiti (redio na televisheni) magazeti, hutaacha kuzungumzia maendeleo viwanda duniani kote.
Unapozungumzia mambo haya yote utaona kwamba ni mambo yenye faida kubwa katika kurahisisha maisha ya mwanadamu. Hata hivyo, pamoja na faida zake, bado maarifa haya yamemtinga kiasi cha kuhatarisha uhusiano wa mwanadamu na Mungu, yamegeuka na kumfanya aende mbio huko na huko.
Hivi sasa mwanadamu muda haumtoshi, yupo ili ayatumikie maarifa wakati mwingine bila yeye mwenyewe kujua, anayatumikia maarifa ili yamnufaishe wakati wote wa uhai wake awapo duniani.
Daniel aliona, akatabiri habari za mambo amabyo yangetokea katika wakati ambapo ameondoka duniani. Alitabiri kuongezeka kwa maarifa duniani, weka hapo kila aina maarifa, kuanzia nyanja za usafiri kama vile meli zinazotumia teknolojia za kisasa, ndege, treni za umeme na magari, kumbuka wakati anatabiri mambo haya hayakuwepo wakati wake.
Sasa yametimia, na yanaendelea kutimia kwa kasi ya ajabu sana, Daniel aliyetabiri hayupo leo, lakini walengwa wa ujumbe huu tupo, tunaishi. Maarifa yamekuja, lakini jambo kubwa limetokea, kwamba hata wale ambao tumeokoka na sisi pia tumetingwa, hatuna tena muda wa kutosha wa kuomba, kulisoma na kulitafakari neno, tuko mbio huko na huko tukiyatumikia maarifa ya ulimwengu huu ili nayo yatunufaishe. Ili tule, tuvae, tujenge, tuendeshe magari, tusomeshe watoto shule.
Utawasikia wanadamu wanaamka asubuhi na mapema, wanajiandaa na wanaaga, wanaenda kazini, wengine kwenye makampuni, viwanda na kwingineko. Maarifa yameongezeka, na yanamhitaji mwanadamu ayatumikie kwa bidii, la sivyo ataishia kuwa masikini.
Katika kuyatumikia ndio maana si ajabu kukuta hata Wachungaji wanaochunga makanisa huku wakiwa wafanya biashara wakubwa tu, au wengine wakiwa wanamiliki makampuni makubwa pia, au ni wafanyakazi katika makampuni na mashirika mbalimbali.
Sipo hapa kupinga au kuunga mkono mambo haya, nakuonyesha namna ambavyo wimbi hili la maarifa lilivyozoa wengi, kaa ukijua kuwa ni Wachungaji ambao kondoo wanangoja malisho kutoka kwao. Hawa watumishi wa Mungu wanaomiliki makampuni au waajiriwa wa mashirika wanahitajika katika vikao vya kampuni zao, na wakati huohuo wanahitajika kuongoza maandalizi ya semina, ibada na mikutano ya kiroho….jaza mwenyewe itakuwaje hapo, tunayatumikia bila kujua.
Angalia huo mchoro hapo juu, maarifa (shuguli za dunia hii) yakimtinga mwanadamu anaweza akakosa ufalme wa Mungu au akaupata, inategemea na vile alivyojiweka, vile alivyokubaliana na hali ya sasa.
Lengo la Malaika yule aliyesema na Daniel kuhusu kuongezeka kwa maarifa si kuturingishia maarifa hayo ambayo yangetokea, lakini alitaka tujue kwamba kuongezeka wa maarifa haya ni ishara moja wapo tunapokaribia ule mwisho wa historia ya maisha ya mwanadamu duniani, siku ambayo KANISA LITANYAKULIWA, yaani wale watu waliokubali kumfuata Kristo na kujikana kwa namna zote.
Malaika yule alimtajia Daniel kwamba maarifa haya yangetokea katika siku za mwisho, wakati wa kumalizia, kwamba kuongeza kwa maarifa haya kutatokea wakati ule ambapo mwisho wa mambo yote utakapokuwa unakaribia kutokea, hii ina maana kwamba, anayetaka kujua Nyakati za mwisho zikoje basi azingatie dalili hii ya kuongezeka kwa maarifa.
Mungu wetu ni mzuri, hajachoka kusema na wanadamu akiwatumia watumishi wake mbalimbali. Muone Paulo anavyosema hapa, 2Timotheo 3:1 “Lakini ufahamu neno hili, ya kuwa siku za mwisho kutakuwako Nyakati za hatari”
Narudia tena, kwamba kama kungekuwa na lugha rahisi zaidi ningesema na wewe kuhusu ujumbe huu. Paulo naye anazungumzia habari ya siku za mwisho, yeye anaeleza kwamba kutakuwako na Nyakati za hatari.
Ni vizuri ikaeleweka hapa kwamba, Paulo hasemi “siku ya mwisho” anasema “siku za mwisho”. Hii ina maana kwamba, kabla ya tukio lile la kunyakuliwa kwa Kanisa, yaani wakati unyakuo utakapokuwa unakaribia, kutatangulia matukio mfululizo yasiyokuwa ya kawaida, matukio au siku za kuogofya hasa kwa waamini halisi.
Kwenye tafsiri moja ya kiingereza, katika mstari huu umetafsiriwa hivi; “katika siku za mwisho itakuwa ni vigumu kwa watu kushikilia imani” hii haina maana kwamba hakuna atakayeweza kushikilia imani yake au kuendelea kuwa Mkristo, hii ina maana kwamba watu wataendelea kushikilia imani zao lakini katika mazingira magumu sana.
Kwa mfano: kuendelea kushikilia imani wakati umefukuzwa kazi na watoto wanalala njaa, au biashara yako ngumu, wateja hamna, wakati huohuo watoto wanahitaji ada ya shule, na pembeni kuna pesa nyingi tu, lakini ili kuzipata ni lazima umkosee Mungu.
Katika mazingira kama haya wengine wameisaliti neema, wenye macho ya kiroho huona chanzo cha maisha yao kuwa magumu, masomo na biashara zao kuwa ngumu, huendelea kung’ang’ana kwa YESU.
Msisitizo:
Nimetangulia kusema kwamba maarifa ni kama vile mfupo wa kibenki, nyanja za usafiri, mawasiliano, ni wachache watakaobaki kwenye sghuli ya asili ya mwanadamu, yaani kilimo. Mashamba nayo yanashikiliwa na baadhi ya matajiri wasiomjua Mungu. Unaweza ukasema tufanye maombi waokoke, lakini kama wapo ili kutimiza unabii sisi wanadamu hatuna cha kufanya, muda wa kuomba matajiri hawa waokoke tungeutumia kuomba neema ya Mungu juu yetu ili tuweze kushinda na kupita kipindi hiki cha mpito wakati Mpinga Kristo anapoandaliwa ili afunuliwe, awe halisi!
Kwa hiyo, wale ambao wengesema wanataka kwenda kwenye kilimo, huko nako kumevamiwa, heri ya wale wacha Mungu ambao hawajauza na hawatauza mashamba yao ili kuwasitiri Watakatifu wa Mungu baadae, labda kama serikali itawataka wauze kilazima. Hilo nalo lisitusumbue, kwa sababu serikali nyingi duniani zipo kumwandaa mpinga Kristo.
Machozi ya Kanisa la leo
Kama kuna kipindi ambacho Kanisa linapaswa kuwa na umakini wa hali ya juu na maombi mazito, basi ni zama hizi za utandawazi, za ubepari, zama za kubinafsisha mali za umma, mali ambazo ziliwafaidisha wote, sasa zinawafaidisha wachache, miongoni mwao ni wale wanaoandaliwa kuwa mawakala wa namna 666.
Nawaambia iliyo kweli, kwamba kama kuna ombi ambalo Kanisa la Mungu linapaswa kuomba kwa mzigo na machozi zaidi katika zama hizi za uovu basi ni MACHO NA MASIKIO YA ROHONI.
Kuna mambo yanaendelea duniani na ndani ya Kanisa la Mungu. Yanaendelea kwa kasi kubwa na ya ajabu sana. Watu wamepokea mambo ambayo yanaitwa maarifa na maendeleo, Kanisa linasema linaenda na wakati, lakini katika mambo hayo ambayo wanasema ni kwenda na wakati ndiyo yale Paulo aliita NYAKATI ZA HATARI. Mambo ambayo yanawafanya watu wamkosee BWANA wakidhani wanamfanyia ibada.
Nimetangulia kusema kwamba lengo la Malaika yule aliyesema na Daniel kuhusu kuongezeka kwa maarifa si kuturingishia maarifa hayo ambayo yangetokea, lakini alitaka tujue kwamba kuongezeka wa maarifa haya ni ishara moja wapo tunapokaribia ule mwisho wa historia ya maisha ya mwanadamu duniani.
TUNAHITAJI MACHO YA KIROHO: Shetani anahakikisha usiku na mchana tunakosa macho, hatuoni yale anayoyafanya dhidi yetu. Anachofanya, anaunda vitu au mambo ambayo ukiyaona yanafanana kabisa na Uungu au Utaua, kama ni nyimbo zote zitamtaja Yesu ili kuficha uwakala wao wa kuzimu, wataimba jina la Yesu na kusema uokoke huku wao wakivaa kama Makahaba, wakinengua na kukata kiuno kama wana wa dunia hii, ili kesho na kesho kutwa uvae na ukacheze kama wao, wenye macho ya kiroho wanayaona haya rohoni, hatukubaliani nao kamwe!
Kama ni mahubiri watahubiri, watahubiri hata kutoa cheche za moto mdomoni, watatenda miujiza mikubwa nay a kutisha, lakini watatembea na waume na wake za watu, watatembea na mabinti ambao ni washirika wao. Wananunua nguvu za kutenda hayo kutoka kwa Ibilisi, watahubiri sana, lakini hawatakuwa na ujasiri wa kukemea dhambi, ni mawakala wa kuzimu hawa, wako kazini, kwa kujua au kutokujua, unahitaji macho ya kiroho, omba, lilia macho haya kwa BWANA, yeye ni mwaminifu, atakupa tu.
Ashukuriwe BWANA YESU aliyetuasa mapema, akasema “mtawatambua kwa matunda yao”. Ajabu ni kwamba, matunda ya kazi hizo potofu yanaonekana, lakini bado baadhi ya Wakristo wanayakumbatia na kuyashangilia. Ukiwauliza watakwambia “mbona wanamtaja Yesu?” au “Mbona wanatenda miujiza?”
Ndugu zangu, tuko katika Nyakati za mwisho, Nyakati za hatari, shetani yuko kazini, anajua kabisa kwamba wakati wake ni mchache uliobaki kabla hajahukumiwa milele. Ufunuo wa Yohana 12:12. Anafanya mambo mengi kwa hila ili kuwarubuni wateule. Kuutambua uongo wa shetani ndani ya Kanisa kunahitaji macho ya rohoni, kwa sababu ni vigumu sana kutofautisha kati ya jambo la Mungu na lile la Shetani.
Uwe makini na mambo yanayoingizwa makanisani yakidhaniwa kuwa ni maendeleo, Neno la Mungu ndicho kioo chetu, angali usije ukazolewa na wimbi hili la hatari.
Watatokea Wahubiri wenye majina makubwa, watajipa majina ya kutisha ili tudhani wametoka Mbinguni jana, lakini bado ni binadamu wenzetu, wanaishi mitaa tunayoishi sisi, wanaendesha magari ambayo hata majambazi wanaendesha, wanakula vyakula ambavyo hata walevi na wazinzi wanakula, lakini wameshindwa kulinda heshima ambayo Mungu amewapa, wakageuka na kuwa mawakala wa kuzimu.
Ndio maana wameruhusu wanawake kuvaa mavazi yoyote, hata yale yasiyositiri miili yao, ukiwauliza wanasema Mungu haangalii mwili, anaagalia roho tu, wataongeza na kusema hata Wazungu waliookoka wanavaa vimini na nguo za uchi makanisani, lakini wanasahau kwamba Wazungu hawa hawana Mbingu za kutupeleka sisi Watanzania au Waafrika, kila mtu atalibeba furushi lake mwenyewe.
Tena, hakuna Injili ya Marekani, Ulaya wala Afrika, ipo injili moja tu nayo ni Yesu Kristo kupitia Biblia. Waseme leo kama Mungu ametuma Biblia iliyoandikwa upya Ulaya. Hapana!! Wenye macho ya rohoni wameona, huu ni ujanja wa Ibilisi akitumia wale wanaojiita Mitume na Manabii kulipotosha Kanisa. Wenye Macho ya kiroho tumesema HATUDANGANYIKI!
Shetani anakazana ili kutupatanisha na Ulimwengu, ili tuwe marafiki wa dunia hii, ukiwa na macho ya kiroho utakataa, hata kama yana nguvu kiasi gani yanapotuvuta tusichoke kupambana, Bwana Yesu karibu atakuja, vumilia kidogo tu, tutaondoka! Usichoke, usije ukakubaliana na dunia hii ukakosana na Mungu, bado kidogo tu BWANA WETU ATARUDI!
Huu sio wakati wa kukubali kila jambo, YESU ANARUDI, na kwa sababu shetani anajua hilo, anafanya bidii kutokosanisha na Mungu.
Yanakuja mambo mengi mbele, amabayo yataonekana si tatizo eti kwa sababu tu yanamtaja Yesu, lakini mwisho wa mambo hayo ni ukengeufu, nasimama katika zamu yangu, nasema hayo mambo yatapokelewa na wengi, lakini ni wenye macho ya rohoni tu ndio watakaosalimika, wale wanaomtafuta BWANA katika mwilikupona kwao itakuwa sawa na ngamia kupenya katika tundu dogo sana la sindano!
Chukizo la Uharibifu linakwenda kusimama patakatifu, lakini baadae atakuwa wazi! YESU ANARUDI!
Simu: 0713 550 778, 0762 822 093
No comments:
Post a Comment